Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

STAMIGOLD Company Limited

BODI YA WAKURUGENZI YA STAMIGOLD YAFANYA ZIARA NA KIKAO MGODINI TAREHE 15 NOVEMBA 2024.

Bodi ya STAMIGOLD inayoundwa na wajumbe sita na mwenyekiti wao ilifanya ziara muhimu katika Mgodi wa STAMIGOLD kwa lengo la kufanya vikao vya bodi na pia kutembelea Mgodi ili kuona hali ya uzalishaji. Ziara hii ilikuwa na umuhimu mkubwa kwani iliwasilisha fursa ya kujua changamoto zinazokabili Mgodi na kutoa ushauri wa kuboresha hali ya utendaji kazi.

Katika ziara hiyo, bodi ilikutana na wafanyakazi wote wa Mgodini na kusikiliza maoni, mapendekezo, na matatizo yao. Wafanyakazi walifunguka kwa kina kuhusu mambo mbalimbali yanayohitaji kuangaziwa. Moja ya mambo makubwa yaliyojitokeza ni changamoto ya nguvu kazi (manpower), yaani upungufu wa wataalamu kama vile surveyors, geologists katika kitengo cha Uchimbaji. Wafanyakazi walisisitiza kuwa ni vema kuongeza wataalamu wa kutosha hususani kwenye vitengo vya uzalishaji hii itasaidia kuongeza uzalishaji mzuri.

Pia, suala la maslahi kwa wafanyakazi lilijitokeza kuwa jambo muhimu. Wafanyakazi walieleza kuna haja ya kuwa na mchakato mzuri na wa haki wa kupandishwa vyeo ili kuhamasisha utendaji bora. Aidha, mazungumzo yalijikita pia katika promotion, (Kupandisha madaraja) mshahara wa kumi na tatu, ambapo walieleza umuhimu wa kuongezewa maslahi ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Kwa ujumla, kikao kilionyesha umuhimu wa kusikiliza na kujali maoni ya wafanyakazi katika kuboresha mazingira ya kazi na utendaji wa Mgodi. Hii ni ishara ya utayari wa bodi kufanya kazi kwa pamoja na wafanyakazi ili kuboresha hali ya kazi na uzalishaji katika Mgodi wa STAMIGOLD. Mwenyekiti wa bodi aliahidi yeye na wajumbe wa bodi kwenda kuyafanyia kazi ila alikumbusha kila kitu kinahitaji fedha hivyo wafanyakazi walihimizwa kuendelea kufanya kazi na kuwa na nidhamu kazini, aidha pia kutunza vifaa vipya ambavyo Mgodi umenunua kwa ajili ya kudumu muda mrefu.