Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

STAMIGOLD Company Limited

STAMIGOLD YASHIRIKI ZOEZI LA UPIMAJI VIRUSI VYA HIV, KUADHIMISHA SIKU YA UKIMWI DUNIANI

Tarehe 1 Desemba inatambuliwa kama Siku ya Ukimwi Duniani, siku muhimu inayolenga kuongeza uelewa kuhusu virusi vya ukimwi (VVU), kupunguza unyanyapaa, na kutokomeza maambukizi ya virusi hivi duniani kote. Katika kuadhimisha siku hii, jamii mbalimbali, pamoja na sehemu ya sekta binafsi, zinaendelea kuchukua hatua za kuhamasisha upimaji na kujua hali ya afya.

Wafanyakazi wa STAMIGOLD wanashiriki kwa wingi katika zoezi la upimaji virusi vya ukimwi (VVU) linaloendelea katika Kliniki ya Mgodi. Zoezi hili ni sehemu ya juhudi za kudumisha afya bora na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa upimaji wa VVU kama njia ya kujua hali ya afya na kuchukua hatua stahiki za kujikinga

STAMIGOLD Inasisitiza kuwa upimaji ni hatua muhimu kwa kila mmoja kujua hali yake ya afya, na pia ni njia mojawapo ya kupambana na maambukizi mapya ya VVU. Kampuni inaendelea kutoa mwongozo wa elimu na kuhamasisha wafanyakazi katika kuchukua hatua zinazofaa kama vile matumizi ya kinga na kupima mara kwa mara, Kutokushiriki ngono zembe, kuwa na mpenzi mmoja, kutochangia vitu vya ncha kali na kupata ushauri wa kitaalamu ili kuzuia maambukizi mapya.

Kwa kuungana na dunia nzima katika kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani, STAMIGOLD imeonyesha mfano mzuri wa ushirikiano katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI, na kuhamasisha wafanyakazi wake kuchukua hatua zinazoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.

"Tujitokeze Kupima, Tuchukue Hatua, Tuzuie Maambukizi!"